Na Reuben Kigame
Nimeshangazwa, kuhuzunishwa na kughadhabishwa na swala zima la mswada huu na imebidi niandike kwa lugha ya nyumbani ndiposa kila mkenya anielewe na pia ajiamulie mwenyewe kama atakubali yanayopendekezwa au la.
Kuna shida nyingi mno na mapendekezo ya serikali kukata asili mia 3 ya mshahara wa kila muajiriwa na mchango wa kiwango hicho hicho kutoka kwa kila muajiri kufidia mpango wa nyumba zinazojengwa na serikali ili kupunguza ukosefu wa nyumba za kuishi nchini.
Maswali ni mengi lakini acha niulize 10 kwa sasa:
1. Ujenzi wa hizi nyumba za bei rahisi unaendelea tayari bila idhini ya waajiriwa na waajiri. Tunaambiwa kwamba kutakuwa na ushirikishi wa waajiri na waajiriwa ili kutahmini kama kufanya hivyo ni sawa au si sawa. Je, kuhusishwa kwa wananchi na waajiri kunaweza kufanyika vipi wakati mradi wa ujenzi unaojadiliwa unaendelea tayari? Ni ujinga wa sampuli gani kwaambia wakenya watahusishwa wakati serikali inajua hawatahusishwa, kisan a maana mradi wenyewe umekwisha kuzinduliwa? Rais ameanzisha ujenzi huo tayari. Isitoshe, wabunge kadhaa kutoka mrengo wa serikali wamesikika wakisema punde mswada utakapofika bungeni wataupitisha kwa sababu rais ana makusudi mazuri ya kumsaidia mwananchi. Hivi inamaanisha kwamba, mpende, msipende, nyumba zitajengwa na fedha zetu zitakatwa.
2. Hoja hii ya kukata pesa za waajiriwa ili kugharamia mradi wa nyumba ilikuwa imeletwa mwaka wa 2018 na serikali ya Uhuru na Ruto na ukakataliwa. Mashirika ya kuwawakilisha wafanyikazi yalipinga mswada huo. Wakati ule kiwango cha kukata mshahara kilikuwa kimekadiriwa kuwa asili mia 1.5. Wabunge na viongozi kwa jumla akiwemo mshauri mkuu wa serikali wa sasa kwa maswala ya fedha, Bw David Ndii, wakisikika kusema pendekezo hilo lingekuwa mzigo mkubwa kwa mwananchi na hasa waajiriwa. Wengi wakajiuliza itakuaje kila mfanyikazi atakatwa hizo hela lakini nyumba kujengwa katika maeneo Fulani Fulani. Kwa kifupi, mpango huo ulikataliwa wakati hela za kukatwa zilikuwa asili mia 1.5. Yapataje kwamba kukatwa asili mia 1.5 mwaka wa 2018 kulikataliwa lakini asili mia 3 inakubalika sasa na serikali na pia mwananchi analazimishiwa mzigo mkubwa Zaidi ya ule mzigo wa 2018?
3. Je, kuna mashirika mengi ya kibinafsi ambayo yameekeza katika ujenzi wa nyumba na mengine ambayo yanatoa mikopo tayari kwa wananchi wanaotaka kumiliki nyumba. Yakuaje serikali haitaki kuongeza idadi ya waekezaji wa kibinafsi, na badala yake, serikali inajiingiza kwa biashara za nyumba kwa kuchukua fedha zawaajiriwa na waajiri kwa lazima?
4. Je, ikiwa mfanyikazi tayari ako na nyumba au tayari yuko kwenye mpango wa kulipia nyumba kwa mashirika ambayo tayari yanajihusisha na ujenzi wa nyumba, yaani mortgage, mbona serikali imkate asili mia 3 kwa lazima ili kugharamia nyumba za wengine?
5. Serikali itatumia mbinu gani kuamua atakayepata nyumba na yule hatapata baada ya mradi wenyewe kukamilika? Isitoshe, kwa sababu ujenzi wa nyumba za bei rahisi umekuwa ukiendelea bila idhini yetu kwa mda, ni wangapi wamefaidika tayari na nyumba zilizokamilika na, je, ni mbinu gani zilitumika kuamua atakayepata na yule hatapata? Tena, ni vyema kufahamu, ni kiwango gani cha fedha kilichoekezwa katika nyumba zilizokamilika tayari na zilitoka wapi ambako zingine haziwezi kutoka?
6. Je, ni utu gani kwa serikali ambayo inaweza kumuangalia mwananchi ambaye tayari anaktwa ushuru wa asili mia 52 nakuongezea kumkata asili mia 3 ya ujenzi wa nyumba, kisha asili mia 2.7 ya NHIF, halafu umpandishie ushuru wa mafuta kutoka asili mia 8 hadi asili mia 16, bila kujali atabaki na nini kukidhi Maisha? Ni unyama wa aina gani huu? Hebu fikiria; ikiwa mwananchi anapata mshahara wa shilingi 10,000 halafu umkate shilingi 5,200 kisha umuongezee mswada kama huu, tofauti yako na mwizi wa mabavu nig ani? Tofauti ya serikali na waporaji nig ani kwa jambo hili?
7. Ikiwa mwananchi ana shida ya kupata chakula na maji, vitu ambavyo humpa uhai, kisha umwambie kwamba unamjali sana kiasi cha kuhusika na atakakoishi kuliko kuwa hai, utakuwa unatumia akili gani? Au niulize, hii ni hekima au ujinga na ushenzi? Ikiwa itabidi uamue kama wananchi watakuwa hai au watapata mahali pa kulala, utaanza na lipi?
8. Serikali kupitia kwa Rais imesema kuwa kukatwa kwa asili mia 3 ya mishahara ni njia ya serikali kumsaidia mwananchi kuokoa hela kupitia uezekaji. Ninauliza, tangu lini ikawa uekezaji unafanywa kwa lazima? Ninayojua kama Kigame ni kwamba ni ushuru tu ambao huchukuliwa kwa lazima au kupitia sheria. Tangu lini savings zikawa za kukatwa hela kwa lazima kupitia sheria? Isitoshe, ikiwa ni kuekeza, je mbona serikali haisemi ni marupurup ya kiasi gani yatakayopatikana au kupewa wananchi watakaokatwa hela hizi? Na pia, je, ni nani atakayepewa marupurupu haya baada ya miaka 7 inayozungumziwa? Ni mwananchi au ni
serikali itakayochukua? Isitoshe, ikiwa kuna wananchi ambao tayari wanaekeza kwa benki na SACCO mbona kuwalazimisha kuekeza kwa serikali?
9. Mwaka uliopita tarehe 24 Oktoba, serikali kupitia kwa mtandao na vyombo vya Habari ilisema kuwa ilikuwa tayari imepata ahadi ya bilioni 500 kutoka kwa mashirika ya kibinafsi kusaidia uekezaji wa nyumba za bei rahisi unaotozwa mwananchi sasa kwa lazima. Je, mbona serikali isiendelee na kuwahimiza waekezaji wa kibinafsi kufadhili mradi huu? Pia, hizo bilioni 500 ziko wapi? Zimetumika vipi? Na nani? Kwa miradi gani?
10. Kwa mda sasa, wananchi sehemu za
mashambani wamekuwa wakijijengea nyumba zao tangu jadi. Mbona serikali haingezungumza na waekezaji kuanzia ufadhili wa nyumba kule mashinani hasa kwa wale ambao hawana makazi? Mbona hatukuanza na utafiti wa kufahamu maskini wa kweli ambao wanahitaji nyumba kabla kuzindua mradi huu, na mbona mijini kuliko vijijini? Tena, mbona walioolewa na wanaishi kwa nyumba za waume wao wakatwe pesa za makazi?
Mnisamehe kwa kuuliza maswali mengi ila niseme hivi. Serikali yetu imekosa muelekeo kama gari lililopoteza control na kuingia kando ya barabara. Serikali yetu imekosa Imani ya wananchi kutokana na ubadhirifu wa fedha, uongo, kutojali na utumizi wa mamlaka vibaya kwa kuwalazimisha wananchi kufanya mambo yatakayoendelea kuwafinya Zaidi. Serikali yetu imekosa utu.
Imekosa kumtendea mwananchi haki. Imekosa maadili na haiaminiki. Serikali yetu haiendelezi ugatuzi kwa mpango huu wa nyumba kwa sababu mradi huu utawafaidi wachache wanaoishi mijini. Pia, wabunge wetu wamekuwa vibaraka vya kutimiza matakwa ya serikali badala ya kuwaaikilsha wananchi waliowachagua. Wabunge wameanza kudhihirisha ujinga wa kufanya itakavyo serikali badala ya kutumia akili na sheria. Isitoshe, wabunge wana majukumu ya kubuni sheria na mikakati ya kboresha Maisha yam wananchi na kumteteakutokana na sheria na sera potofu, ila wamegeuka kuwa “wafuata nyayo” za ikulu. Wanasheria, wasipoangalia, nao pia watakuja kufanyika vibaraka kama hivi.
Ni jukumu la kila kiongozi kuweka maslahi yam wananchi mbele, n ani jukumu la kila mwananchi kukataa sera na sheria zo zote za kumkandamiza na kumuumiza. Haina haja kabisa kulazimishiwa viongozi na sera za kuumiza badala ya kurahisisha Maisha. Katiba katika ibara ya 1 inasema mwananchi ndiye aliye na uwezo mkubwa katika nchi. Yapataje tunavumilia viongozi – ndugu zetu waliozaliwa kama sisi hapa – kutuongoza kimabavu na kutunga sera na sheria za kutuzika tukiwa hai?
Nimalizie kwa kusema kuwa viongozi wo wote wanaoenda kanisani au misikitini kila juma inawapasa kujiuliza kama Mungu anapendezwa na wachache kufaidika weingi wakiumia. Ni Mungu gani huyu ambaye anaabudiwa na viongozi wetu ambao hawataki kusoma jinsi Mungu anataka wananchi kushughulikiwa? Ni Mungu gani huyu anayefurahishwa na rushwa, ukabila, mauaji, uongo, ukora, na kutojali wengine?
Tafakari hayo kwa sasa.